ZANZIBAR
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar jana imetoa tamko la kusitishwa rasmi kwa zoezi la utafutaji wa miili ya watu walionasa kwenye vyumba vya meli ya MV Spice Islander iliyozama eneo la Nungwi Kaskazini mwa Kisiwa cha Unguja huko Zanzibar kutokana na ugumu wa utekelezaji wa zoezi hilo.
Afisa Habari wa Jeshi la Polisi Zanzibar Inspekta Mohammed Mhina, amesema kuwa kusitishwa kwa zoezi hilo kunatokana na kushindwa kwa wazamiaji wa Kimataifa kutoka nchini Afrika ya Kusini kuifikia meli hiyo kutokana na kina kirefu kilichopo eneo la ajali pamoja na hali mbaya ya hewa.
Akitangaza uwamuzi huo wa Serikali, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Idi, amesema kuwa ingawa Serikali ilikuwa na nia ya kutaka kutolewa kwa kila mwili ulionasa kwenye meli hiyo, lakini imeonekana kuwa zoezi hilo ni gumu kutekelezeka.
Amewaomba Watanzania kukubali kuwa ndugu zao waliopoteza maisha na miili yao kushindindikana kupatikana, ni mapenzi na maamuzi ya Mwenyezimungu aliyeamua kuwa bahari iwe sehemu ya makaburi ya ndugu zetu hao.
Balozi Idi amesema kila mmoja hana budi ya kumshukuru Mungu na kukubaliana na hali hiyo kwani amesema hata kama Serikali ingekuwa na nia ya kuendelea na zoezi hilo, lingechukua muda mrefu na mwisho wa siku huenda pia mafanikio yasiwepo.
Lakini pia Balozi Idi, amesema tangu kuzama kwa meli ya Spice Islander hadi leo ni muda mrefu kiasi ambacho hata kama miili ingefanikiwa kutolewa isingekuwa rahisi kutambulika kutokana na kuharibika vibaya.
Katika hatua nyingine Balozi Idi amesema kuwa taarifa zote zinazohusu tukio hilo zitatolewa na ofisi yake ama kupitia kwa Waziri wa nchi katika ofisi yake Mh. Mohammed Aboud ili kuepuka utoaji wa taarifa za kuwachanganya wananchi.
No comments:
Post a Comment