Monday, September 12, 2011

Mbowe atua Zanzibar kuzungumzia ajali ya meli


DAR ES SALAAM

Mwenyekiti wa Taifa wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe, amewasili Zanzibar kufuatia kutokea ajali mbaya ya meli usiku wa kuamkia Jumamosi inayokisia kuuwa zaidi ya watu 200.

Taarifa kutoka Zanzibar zinasema kuwa Mbowe, ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni na Mbunge wa Hai, amepanga kukutana na waandishi wa habari kwenye hoteli ya Serena muda wa saa 3 asubuhi leo hii siku ya Jumatatu.

"Mbowe anatariwa kutoa mkono wa rambirambi kwa wananchi wa Zanzibar kutokana na msiba huu mkubwa wa kitaifa," kiongozi mmoja wa CHADEMA aliiambia Tanzania files.

"Pamoja na kutoa rambirambi, Mbowe pia anatarajiwa kutema cheche na kuzisulubu serikali za Zanziba na muungano kutokana na uzembe mkubwa uliosababisha kutokea kwa tukio hilo."

Zaidi ya watu 600 waliokolewa kwenye ajali hiyo ya meli ya "MV Spice Islander." Uchunguzi wa awali umeonesha kuwa chanzo cha ajali hiyo ni meli kutokuwa kwenye hali ya usalama na kuzidishwa kwa idadi ya abiria na uzito wa mizigo kuliko uwezo wa chombo chenyewe.

CHADEMA ndiyo chama kikubwa cha upinzani nchini Tanzania. Hata hivyo, chama hicho hakina nguvu kubwa ya kisiasa na ushawishi Zanzibar.

Kitendo cha Mbowe kwenda Zanzibar na kuzungumza na wananchi kupitia vyombo vya habari kuhusu ajali hiyo ya meli kimetafsiriwa na wadadisi wa masuala ya kisiasa kuwa ni mtaji mzuri kwa CHADEMA kujichotea wafuasi zaidi Zanzibar.

"Pamoja na jitihada za CHADEMA, vyama vya CCM na CUF vitaendelea kutawala siasa kwenye visiwa hivi kwa miaka mingi ijayo kutokana na masuala ya kihistoria, utamaduni na dini," alisema afisa mmoja aliye karibu na serikali.

Wakati huohuo, Mohamed Mhina wa Jeshi la Polisi Tanzania anaripoti kutoka Zanzibar kuwa wazamiaji 12 kutoka nchini Afrika ya Kusini waliwasili Zanzibar Jumapili usiku kuungana na wazamiaji wengine wa vyombo vya ulinzi na usalama hapa nchini.

Wataalamu hao kutoka Afrika Kusini wamewasili ili kufanya uhakiki wa kujua kama bado kuna mili iliyokwama kwenye meli hiyo.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mohamed Aboud, amesema kuwa wazamiaji hao wamewasili wakiwa na zana za kisasa za uzamiaji na kwamba kazi ya kwanza itakayofanywa na timu hiyo ni kuhakikisha kuwa wanaifikia meli hiyo iliyozama umbali wa karibu nusu kimometa kwenye mkondo mkubwa wa maji na majabali.

Bado Serikali na wananchi mbalimbali wanadhani kuna miili ya watu waliokwama katika vyumba vya meli hiyo tangu ilipozama usiku wa Jumamosi Septemba 10 mwaka huu ikiwa na idadi ya watu isiyojulikana.

Makundi ya wananchi wamekuwa wakitaja idadi ya ndugu na jamaa waliosafiri na Meli hiyo na ambao hawajapatikana wakiwa hai ama miili yao kiasi cha kutia shaka kuwa huenda bado wamenasa ndani ya vyumba vya meli hiyo iliyozama chini ya kina kirefu cha mkondo wa bahari ya Hindi.

Tangu kuokolewa kwa abiria 619 na kuopolewa kwa miili ya watu 197 hadi Jumamosi jioni, hakujapatikana mtu hai ama mwili wa abiria aliyekufa maji ukielea juu ya maji ama kukokotwa kupelekwa mwambao mwa nchi kavu.

Katika eneo ilipozama Meli hiyo zipo Meli nyingine za MV Kasa ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania pamoja na MV Mamba ya Jeshi la Polisi ambazo zote ziliwasili alfajiri siku iliyotokea tukio hilo la kuzam,a kwa MV Spice Islander.

No comments:

Post a Comment